TRA KAGERA YATOA ONYO JUU YA HATARI ZA MAGENDO

Na Lydia Lugakila, Bukoba

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera imeonya vikali kuhusu hatari zinazotokana na uingizaji wa bidhaa nchini kwa njia ya magendo, na kueleza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika. 


Onyo hilo limetolewa na meneja wa TRA mkoa wa Kagera, Castro John, kupitia taarifa aliyotoa kwa umma.


Castro amesisitiza umuhimu wa wananchi wa Kagera na maeneo jirani kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vya magendo vinavyokiuka sheria za forodha. 

Casto amesema, "Vitendo vya magendo si tu ni makosa ya kisheria, bali pia vinaweza kuhatarisha usalama wa jamii, kupunguza mapato ya serikali, na kuathiri huduma muhimu kama elimu, maji, na afya."


Aidha Meneja huyo amewataka wale wote wanaojihusisha na biashara haramu za magendo kuacha mara moja, ambapo amesisitiza kuwa wahusika watakaokamatwa watawajibika kulipa faini, na bidhaa zao zitakamatwa na kesi zao zitaelekezwa mahakamani.


TRA pia imewakumbusha wananchi kutumia vituo rasmi vya forodha vilivyopo mipakani, kama vile Mutukula, Murongo, Kabanga, Murusagamba, Rusumo, Kanyigo, pamoja na bandari za Kemondo na Bukoba kwa ajili ya uingizaji na uondoshaji wa bidhaa.


Meneja wa TRA ameongeza kuwa wote wenye magari yenye usajili kutoka nchi jirani wanapaswa kuyawasilisha katika ofisi za forodha za Mutukula, Kabanga, Rusumo, na Bukoba ili kufanyiwa taratibu zinazostahili, ikiwa ni pamoja na malipo ya kodi na usajili.


Castro amewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya magendo, huku akisisitiza atakayetoa taarifa za kufichua vitendo vya magendo watapewa zawadi ya asilimia tatu ya kodi itakayokusanywa.

Chapisha Maoni

0 Maoni