KAMENGE AWASHAURI VIONGOZI KUWEKEZA KATIKA ELIMU YA KILIMO KWA VIJANA BADALA YA KUWAPELEKA BUNGENI KUTAMBULISHWA KAMA WAGENI

Na Lydia Lugakila

Kagera

Katika kipindi hiki ambacho vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, ni muhimu kuangazia jukumu la viongozi mbali mbali wa Taifa hili katika kusaidia kundi hili muhimu la jamii badala ya kupeleka vijana 25 hadi 30 Bungeni ili kushuhudia shughuli za kisiasa.


Kauli hiyo imetolewa na mchumi na mkulima kutokea mkoani Kagera Evance Kamenge wakati Akizungumza na Waandishi wa habari waliotaka kujua masuala mbali mbali ya kilimo kwa vijana wa sasa.

Evance amesema kuwa wanahitaji viongozi ambao watachukua hatua za kuwasadia vijana kuelewa na kuboresha sekta ya kilimo.


"Mimi ni mkulima wa kahawa na ndizi hapa Bukoba, nasikitika kuona wenzangu wengi wakikumbwa na maumivu kutokana na ukosefu wa elimu sahihi kuhusu kilimo hivyo tunahitaji viongozi ambao watakuja na kutoa elimu kuhusu mbinu bora za kilimo, kama vile kupanda mihogo na ndizi, ili kuboresha maisha yetu na kuleta maendeleo endelevu" alisema Evance Kamenge.


Mchumi huyo amesema kuwa vijana wengi wanaoendelea na elimu ya juu hawawezi kuajiriwa kila wakati, hivyo ni muhimu kuwaelekeza kwenye fursa za kilimo.


"Kwa mfano, wapo vijana wanaolima na kupeleka mazao kama nyanya nchini China na Australia tunaweza pia kufikia mafanikio kama hayo ikiwa tutapata elimu na msaada wa kutosha katika kilimo" alisema Evance


Ameongeza kuwa ni aibu kuona vijana wakijihusisha na kazi za bodaboda kama njia pekee ya kujikimu, wakati ipo ardhi kubwa na rasilimali ambazo hazijatumika vizuri


Ameeleza kuwa kila kijana anapaswa kuwa na malengo thabiti kuhusu matumizi ya kipato chake.


Aidha ameongeza kuwa  Kijana anayepata pesa kupitia boda boda anapaswa kuongeza malengo yake ajitafutie ardhi na kuwekeza katika kilimo.


"Kijana akiwa na hekari 2 hadi 3 hii itamsaidia kuwa na uhakika wa kesho na kuimarisha uchumi"aliongeza mwanauchumi huyo


Amesema kuwa kijana anapaswa kuona pikipiki kama chombo cha kusafiri kwenda shambani, si kama kazi yake ya kila siku.


Mkulima huyo amesisitiza kuwa , ni lazima viongozi  wawe na mtazamo wa kisasa kuhusu rasilimali za nchi, hususan ardhi.


Amesema kuwa viongozi wanaohitajika ni wale wanaoweza kutunga sera zitakazowasaidia vijana wengi kutoka katika hali ngumu walizonazo na kuhamasisha mifumo ya uchumi endelevu.


"Kama Nchi, lazima tujenge mazingira ambayo yanawezesha vijana kuwa na mawazo na mipango endelevu, ili tuwe na kizazi chenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisasa"alisema Kamenge.


Hata hivyo ameongeza kuwa muhimu kwa wanasiasa kuelewa kuwa kuwapeleka vijana Bungeni si suluhisho. Badala yake, wanapaswa kufanya kazi na vijana, kuwapa elimu, na kuhamasisha shughuli za kilimo ambazo zitawasaidia kujenga maisha bora na endelevu.

Chapisha Maoni

0 Maoni