Na Lydia Lugakila
Evance Kamenge, mchumi na mkulima kutoka mkoani Kagera, amewataka wanasiasa kuacha kuoneana wivu na badala yake wajenge ushirikiano wa karibu na wadau wa maendeleo katika maeneo yao.
Haya yameelezwa wakati Kamenge alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu juhudi zake za kuchangia maendeleo, hasa katika wilaya ya Missenyi.
Katika mahojiano hayo, Kamenge alisisitiza umuhimu wa kushirikiana ili kuharakisha maendeleo katika jamii.
“Wakati wanasiasa wakishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, kuna uwezekano mkubwa wa kuleta maendeleo kwa haraka.
Amesema kukosa ushirikiano kunakwamisha maendeleo na kusababisha matatizo mengi,” alisema Kamenge.
Aliongeza kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakichukulia msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama tishio kwa nyadhifa zao, hali ambayo inawakatisha tamaa wanaojitolea kusaidia jamii.
“Ni muhimu wanasiasa waachane na mtazamo huo na kuzingatia jinsi ya kushirikiana na wadau kwa faida ya wote,” alisema.
Kamenge amewahimiza wanasiasa kuzingatia wajibu wao wa kutumikia wananchi kwa moyo mmoja, huku akisisitiza kuwa ni lazima waanze kutenda kwa ajili ya jamii badala ya kuangalia tu maslahi yao binafsi.
“Wananchi wanahitaji viongozi wanaojali na kutenda kwa ajili yao,” alisisitiza Kamenge.
Wito huu unakuja wakati ambapo changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii zinahitaji mchango wa pamoja ili kufanikisha maendeleo endelevu.
Evance Kamenge anawataka wanasiasa wa Kagera kuchukua hatua zitakazosaidia kuimarisha ushirikiano kwa maendeleo bora ya wananchi.

0 Maoni