Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limesikitishwa sana na linalaani tukio baya la uovu la kuvamiwa, na kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Charles Kitima, lililotokea tarehe 30 Aprili 2025 majira ya saa 4 usiku katika makazi na Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu, Kurasini Dar es Salaam.
Padre Kitima alipata majeraha makubwa na amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es salaam. Tunawashukuru wote waliomsaidia na kumfikisha Padre Kitima hospitalini mapema na kwa madaktari na wauguzi wanaomhudumia mpaka sasa.
Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huu wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, uchunguzi wa tukio hili ufanyike kwa haraka na taarifa zilitolewe kwa uwazi na bila upotoshwaji wowote ili kurudisha imani na matumaini kwa watu wetu.
Tunashukuru mpaka sasa kwa ushirikiano mzuri tunaoupata kutoka Serikalini na kwa vyombo vyetu vya usalama.
Pia tunawashukuru watu binafsi, taasisi za ndani na za kimataifa zinazoendelea kulaani na kutupa pole kwa tukio hili baya na la aibu kwa Taifa letu.
Tunaomba Waamini na watu wenye mapenzi mema muendelee kumuombea neema ya uponyaji Padre Kitima, na pia kuliombea Taifa letu amani na umoja. Aidha, tunawaomba muwe na subira na uvumilivu wakati tukisubiri matokeo ya uchunguzi wa vyombo vinavyohusika.



0 Maoni