Aprili 30, 2025 Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela kijana Hasan Sudi (24), mkazi wa Mtaa wa Simba,Bodaboda,Muha kwa kosa la kumbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 8.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mnamo Novemba 13, 2024 katika mtaa wa Msimba, ambapo mshtakiwa, ambaye ni mwendesha bodaboda maarufu eneo hilo, alitenda kosa hilo la kikatili dhidi ya mtoto wake wa kumzaa.
Akitoa hukumu hiyo Mheshimiwa Hakimu Kahungu alisema kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka uliithibitishia mahakama bila shaka kwamba mshtakiwa alihusika na kitendo hicho.
Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa alitumia nafasi yake kama mlezi kumdhuru mtoto huyo, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kibinadamu na kisheria.
Katika hukumu yake, Mheshimiwa Kahungu alisisitiza kuwa adhabu hiyo iwe fundisho kwa wazazi na walezi wote wanaojaribu kutumia mamlaka yao vibaya dhidi ya watoto.
Mamlaka zimeendelea kuhimiza jamii kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia na kuhakikisha watoto wanakuwa salama majumbani mwao.

0 Maoni