DKT. DORIYE ASISITIZA NIDHAMU NA UZALENDO KATIKA ULINZI WA RASILIMALI KWA MAAFISA NA ASKARI WA HIFADHI NGORONGORO

 Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye akizungumza leo tarehe 12 Mei, 2025 baada ya kuwavisha vyeo jumla ya watumishi 621 ikijumuisha Maafisa 145 na askari 476 wa jeshi la Uhifadhi. 

Akizungumza na watumishi hao baada ya kuwaapisha na kuwavisha vyeo Dkt. Doriye amewasisitiza maafisa na askari wa jeshi la uhifadhi kuzingatia kiapo walichoapa na kuzingatia maadili ya utendaji kazi, kuzingatia sheria, ushirikiano, upendo na kujiepusha na rushwa katika maeneo ya kazi.

“Leo mmeapa na kuvishwa vyeo vya kijeshi, mnapaswa kuonesha dhamira ya dhati ya kulinda Hifadhi ya Ngorongoro na rasilimali zote za uhifadhi, vyeo mlivyovishwa vinakuja na majukumu makubwa ambayo yanahitaji kujituma na kuwajibika ipasavyo, hakikisheni mnakuwa mfano bora kwa jamii kwa kuzingatia maadili, nidhamu, sheria, uaminifu, uzalendo kwa rasilimali za nchi, kujiepusha na vitendo vya rushwa na kufuata miongozo ya jeshi la Uhifadhi” alisisitiza Dkt. Doriye.

Aidha Kamishna Doriye amewakumbusha  watumishi hao kuwa, kupanda cheo ni kuongezewa majukumu ya kiuongozi katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi, utalii, ulinzi, maendeleo ya jamii na urithi wa asili na utamaduni uliopo hifadhi ya Ngorongoro na kusisitiza kuwa suala la mafunzo ya kijeshi kwa watumishi wa NCAA litakuwa endelevu ili kuendelea kujenga utimamu wa mwili kwa afisa na askari.


Chapisha Maoni

0 Maoni