Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imemhukumu Selemani Kafukuntu (51) mkazi wa kijiji cha Kasekese Wilaya ya Tananyika kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa darasa la pili mwenye umri wa miaka sita (6)
Hukumu hiyo imetolewa Aprili 09, 2025 mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Mhe. Silivester Makombe.
Akisoma hukumu hiyo Mhe. Makombe alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 09, 2025 huko katika kijiji cha Kasekese kwa kumvizia mtoto huyo akiwa nyumbani kwao anacheza na wenzake kisha kumrubuni kwenda kumnunulia maandazi kisha kumfanyia unyama huo.
Mshtakiwa huyo mara baada ya kutenda tukio hilo alikimbia kusikojulikana ambapo Jeshi la Polisi likifanya juhudi za kumsaka na Januari 15, 2025 alikamatwa.
Mhe. Makombe amesema Mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo chini ya kifungu namba 130 sura ya 16 cha sheria ya kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Kesi hiyo ilikuwa na jumla ya mashahidi watano akiwemo daktari wa binadamu, ambapo Mhe. Makombe alisema mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa pasipo shaka uliotosha kumtia hatiani mtuhumiwa.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 29, 2025 na kusajiwa kwa kupewa namba kesi ya jinai 5272 ya mwaka 2025.
.jpeg)
0 Maoni