Si kila kazi utakayofanya ulimwenguni basi utapaswa kulipwa Pesa, unadhani wazazi wako waliokuzaa na kufanya kazi kubwa ya kukupa malezi bora na kukusomesha wanahitaji kulipwa Pesa...?
Kiuhalisia watu wengi wana Pesa ila ni maskini wa utu na upendo, waliosema Pesa inaongea wakati wa matumizi ndiyo wale wale ambao leo wanasema kuwa pesa ni bubu wakati wanaitafuta...
Walichosahau si kila wakati Pesa ikiongea kila kitu hubaki kimya, kwa sababu vitu vizuri na bora ulimwenguni huwa havinunuliwi, havioekani na wala huwezi kuvigusa kwa mikono yako...
Jitihada inamfundisha mtu kujua thamani ya Pesa wakati wa kutafuta, na matumizi ya hovyo huifundisha pesa namna ya kumkimbia mtu na kurudi ilipotoka...
"Pesa ni kama mwanasiasa tu huwa haina rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu..."
Mzazi bora atamfundisha na kumrithisha mtoto wake nidhamu ya matumizi ya pesa ili aweze kutengeneza na kuzalisha pesa...
Na sio kumrithisha mtoto pesa zitakazokuwa daraja la kumwingiza kwenye umaskini...
Mtoto akishindwa kuifahamu miongozo, kanuni na taratibu za pesa, hufikiri kila kitu ulimwenguni hupatikana ukiwa na pesa na atafikiri kila kitu kinaweza kununuliwa na kuuzwa kama bidhaa au huduma...
Ni vizuri kuwa na pesa na vyote ambavyo pesa inaweza kununua, ila katika mchakato wa kutafuta pesa usikubali kupoteza vile ambavyo pesa haiwezi kununua ili uipate pesa...
Wanasema ni heri ukawa huna pesa lakini una furaha kuliko kuwa na pesa halafu huna amani...
Pesa inaweza kununua mapenzi sio upendo, inaweza kununua kitanda sio usingizi, inaweza kununua saa sio muda, inaweza kununua watu wa kuwa nao karibu lakini sio marafiki...
Pesa inaweza kununua urembo sio uzuri, inaweza kununua nguo sio utanashati, pesa inaweza kununua chakula sio hamu ya kula, inaweza kununua dawa sio afya, na inaweza kununua pete sio ndoa...
Kwa kawaida ilipaswa watu kuomba vile ambavyo hawana ila wengi wanaomba pesa sio kwa sababu hawana ila kwa sababu haitoshi...
Usimwombe Mungu kitu ambacho unacho ila unaona hakitoshi, muombe Mungu kitu ambacho huna na unastahili kukipata lakini kwa uwezo wako huwezi kukipata...
Mfalme Selemani alikuwa na watu akaomba kwa Mungu hekima ili awaongoze kwa haki...hakuomba pesa ili awe tajiri na mwenye mali nyingi...
"Remember NEEDS are much stronger than WANTS..."
☆Mwandamizi


0 Maoni