IDARA YA UHAMIAJI YAPATA MAFUNZO ELIMU YA AFYA.

 


‎ Na. Konstebo Elisha Lusatila - Dodoma

‎ Maafisa na Askari kutoka idara ya uhamiaji wamepata mafunzo juu ya masuala ya uelimishaji rika, Afya ya akili, ukimwi pamoja na magonjwa yasiyoambukizwa.

‎Mafunzo hayo yaliyohusisha mikoa 14 na vituo 3 yamefanyika katika ukumbi wa jeshi la zimamoto makao makuu Dodoma.


‎Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo kamishna wa mafunzo CI Amiru Sadick amesema lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha watumishi wa Idara ya Uhamiaji wafanye kazi wakiwa na afya njema bila kuwa na changamoto zinazoepukika hali ambayo itaongeza weledi katika kazi.

‎Mwezeshaji Bwana Deogratius Sukambi ambaye ni mwanasaikolojia ameelezea jinsi gani watumishi wa umma wanaingia kwenye changamoto ya afya ya akili na chanzo kikubwa ni msongo wa mawazo na masuala ya kiuchumi hivo amewaasa tatizo hili haliui lakini kadiri unavyozidi kukwepa kulitibu ndivyo unazidi kuwa na tabia, maamuzi na magonjwa yatakayokuua.

‎Dkt Hatibu Kachenje kutoka Hospitali ya rufaa mkoa wa Dodoma ametoa elimu juu ya masuala ya UKIMWI na VVU ambapo amegusia vyanzo vya maambukizi ya UKIMWI na jinsi gani ya kuishi na mtu mwenye virusi vya UKIMWI kwani ugonjwa huo hauambukizwi kwa njia ya kugusana hivo amewaasa watumishi kutowatenga wagonjwa hao.

‎ Dkt. Kachenje ameongezea kwa kusema watumishi wapewe elimu mara kwa mara juu ya masuala ya UKIMWI na VVU.

‎ Akizungumza kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa Dkt. Mukhisin Chikota kutoka Hospitali ya rufaa mkoa wa Dodoma amesema njia za kuepuka magonjwa yasiyoambukizwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya vyakula vilivyohifadhiwa kwa kemikali, kula mlo kamili kupunguza matumizi ya chumvi na sukari na kupima afya mara kwa mara Akifunga mafunzo hayo Mkuu wa divisheni ya anuai za jamii SACI Tununasya Ng'ondya amesisitiza huduma ya kwanza ikafanyike kwa weledi na vifaa tiba vitumike na sio vikae bila kuwapatia huduma watu wenye changamoto ofisini,

‎ Pia SACI Ng'ondya ameongezea kwa kumshukuru kamishna jenerali wa idara ya uhamiaji CGI Dkt Anna peter Makakala kwa kuwezesha semina hii ambayo itaenda kuleta mabadiliko kwa wafanyakazi wa idara ya uhamiaji.

Chapisha Maoni

0 Maoni