Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linaendelea kutekeleza majukumu yake sambamba na kuwashirikisha na kushirikiana na wananchi katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu.
Pia linaendelea na operesheni na misako kukabiliana na wachache ambao hawataki kujitafutia kipato kwa njia halali. Aidha Februari 08,2026 majira ya saa nane na nusu usiku katika Mtaa wa NMB Kata ya Malambo, Wilaya ya Bariadi watu watatu waliuawa katika majibizano ya risasi na Askari Polisi.
Tukio hilo lilitokea baada ya Polisi kupokea taarifa kuwa kuna watu wanavunja milango ya jengo la Simiyu Money Services linalotumiwa kutoa huduma za miamala ya fedha ya Makampuni ya simu na Kibenki.
Kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na uhalifu walifika katika eneo hilo na watu waliokuwa wanatekeleza uhalifu katika jengo hilo walipobaini wanafuatiliwa walianza kufyatua risasi jambo ambalo liliwalazimu kujibu mapigo na kufanikiwa kwajeruhi watuhumiwa watatu.
Watuhumiwa hao walipoteza maisha wakati wanakimbizwa hospitali kwa matibabu.
Askari walifanikiwa kupata silaha moja aina ya AK 47 waliokuwa wanatumia majambazi hayo na risasi nane ndani ya magazini.
Pia katika upekuzi walikutwa wakiwa na shilingi mia tatu fedha ya Kenya, noti ya shilingi 5 pesa ya Misri,tiketi ya kutoka Migori kuja Sirari na tiketi za kutoka Sirari hadi Lamadi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linaendelea kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika kubaini na kuzuia uhalifu. Pia linatoa onyo kwa baadhi ya watu wanaendekeza tabia ya kufanya uhalifu kwa sababu hasara yake ni kubwa kwao.

0 Maoni