Kiruswa: “Serikali, Wadau Kukutana Kutafuta Mwarobaini Kero Madini ya Jasi,”

▪️Akemea Jasi Kuuzwa na Kununuliwa Chini ya Bei Elekezi

▪️Aingilia Kati Kero kwa Wachimbaji Wadogo, Wadau Kukutana Dodoma Kutafuta Suluhu ya Kudumu

Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inatarajia kukutana jijini Dodoma katika siku za karibuni na wadau wa madini ya jasi (gypsum) wakiwemo wachimbaji wadogo, wasafirishaji, wamiliki wa viwanda vya saruji, Uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Same ili kujadili na kutatua changamoto zinazoathiri shughuli za uchimbaji na biashara ya madini hayo ambazo zimechangia kusuasua kwa maendeleo ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo.

Alitoa kauli hiyo jana, Desemba 12, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji katika Kata za Makanye na Ruvu Jeungeni, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, ambako pia alizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya jasi.

Dkt. Kiruswa alisisitiza marufuku ya kununua madini ya jasi chini ya bei elekezi iliyotolewa na Tume ya Madini, akiwataka wote kuheshimu miongozo hiyo ili kulinda maslahi ya wachimbaji.

Kwa upande wa mazingira,


alitoa wito kwa wachimbaji kuhakikisha utunzaji wa mazingira, kufukia mashimo mara baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika, pamoja na kupongeza juhudi za uanzishwaji wa Mfuko Maalum wa kusaidia kurejesha mazingira mara baada ya kutamatika kwa shughuli za uchimbaji, ambao umeelezwa kuwa chachu ya kuimarisha uwajibikaji na uendelevu wa shughuli za madini wilayani humo.


Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa aliendelea kusisitiza umuhimu wa mafunzo ya MBT kwa vijana na wanawake, utoaji wa leseni, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa ili kuongeza ufanisi na usalama katika uchimbaji mdogo wa madini ya jasi na kuwahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini.

Chapisha Maoni

0 Maoni