WAZIRI LUKUVI AONGOZA KIKAO KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI

Na Mwandishi wetu-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William  Lukuvi, ameongoza kikao maalum cha maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yanayotarajiwa kufanyika tarehe 1 Desemba 2025.

Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko, na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt. Samwel Sumba.
Pia, baadhi ya Wakurugenzi na Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya TACAIDS walishiriki katika kikao hicho ambacho kililenga kupitia mipango na mikakati ya maandalizi ya kitaifa kuelekea maadhimisho ya mwaka huu.

Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili hatua za mwisho za uratibu, mbinu za kuongeza uhamasishaji kwa jamii, na kuhakikisha kuwa ujumbe wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani unawafikia wananchi kwa ufasaha na kwa wakati.

 

Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hufanyika kila mwaka ili kuongeza mwitikio katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU, kupunguza unyanyapaa, na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa watu wanaoishi na VVU.

Chapisha Maoni

0 Maoni