DOYO AAHIDI SOKO LA KIMATAIFA LA MAZAO KUINUA WAKULIMA WA NYANDA ZA JUU KUSINI

 *WAKATI WA KUBADILISHA KILIMO CHA KUJIKIMU KUWA CHA KIBIASHARA NI SASA

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameahidi kwamba, endapo atachaguliwa kuwa Rais, serikali yake itajenga Soko la Kimataifa la Mazao katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Lengo la mradi huo ni kuwaunganisha wakulima wa eneo hilo na masoko ya bara lote la Afrika, ili kuongeza thamani ya mazao na kipato cha wakulima.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni na wananchi wa Mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga, katika maeneo ya Soko Kuu la Sabasaba, Mhe. Doyo alisema kuwa ujenzi wa soko hilo utakuwa sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuinua sekta ya kilimo na kuongeza tija kwa wakulima wadogo na wa kati nchini. “Serikali yangu itawekeza katika ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mazao Nyanda za Juu Kusini. Soko hili litaunganisha wakulima wetu na bara lote la Afrika, kurahisisha upatikanaji wa masoko yenye tija, na kuhakikisha mazao ya Watanzania yanapata thamani kubwa zaidi,” alisema Mhe. Doyo.

Amesema kuwa Nyanda za Juu Kusini zimebarikiwa kijiografia kutokana na hali nzuri ya hewa na mvua za kutosha, hali inayowezesha kilimo cha uhakika na cha muda mrefu. Aliahidi kwamba serikali yake itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa kilimo cha kisasa watakaoshirikiana na wakulima kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.

Aidha, Mhe. Doyo alisisitiza kuwa ukanda wa Nyanda za Juu Kusini una uwezo mkubwa wa kulisha taifa lote na hata kusafirisha chakula na mazao ya biashara kwenda nchi jirani za Afrika Mashariki endapo mipango madhubuti itawekwa. “Tutahakikisha kila mkulima ana soko la uhakika, ndani na nje ya nchi. Hii itawawezesha kuajiri vijana, kupunguza tatizo la ajira, na kuongeza kipato cha familia,” aliongeza Mhe. Doyo.

Ameeleza kuwa haiwezekani vijana wa Tanzania wakaendelea kukosa ajira ilhali sekta ya kilimo, ikipangwa vizuri, inaweza kutoa ajira nyingi na zenye staha.

Kwa mujibu wa Mhe. Doyo, takribani asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo kama chanzo kikuu cha kipato, lakini asilimia 90 ya wakulima wadogo bado hawatumii mbegu bora, teknolojia ya kisasa, wala pembejeo sahihi kutokana na uwekezaji mdogo katika sekta hiyo.

Akinukuu takwimu za Benki ya Dunia (World Bank, 2022), alisema sekta ya kilimo ilipokea chini ya asilimia 6 ya bajeti ya taifa, kinyume na lengo la asilimia 10 lililowekwa na Azimio la Malabo kwa nchi za Afrika.

Aidha, takribani asilimia 40 ya mazao hupotea kabla ya kufika sokoni kutokana na uhaba wa maghala, barabara mbovu, na ukosefu wa viwanda vya usindikaji. “Serikali ya NLD itahakikisha sekta ya kilimo inapewa kipaumbele. Tutapandisha bajeti ya kilimo hadi asilimia 14 ya bajeti kuu ya taifa, ili kuhakikisha kilimo kinakuwa uti wa mgongo wa uchumi wetu,” alisisitiza Mhe. Doyo.

Kauli ya Mhe. Doyo inaakisi dira yake ya kuimarisha uchumi wa kilimo, kukuza ajira kwa vijana, na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya mazao barani Afrika.



Mpaka sasa, msafara wa mgombea urais huyo wa Chama cha NLD umefanya kampeni katika mikoa 24 na wilaya 78. Kwa sasa msafara huo unarejea tena mkoani Tabora, Shinyanga na Kilimanjaro, kabla ya kuelekea Zanzibar.

Chapisha Maoni

0 Maoni