Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limemshukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kukabidhiwa magari matano mapya kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za ulinzi na usalama katika mkoa huo.
Magari hayo yamekabidhiwa kwa Wakuu wa vitengo mbalimbali mkoani humo leo Septemba 10, 2025, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, SACP Shadrack Masija.
Akizungumza katika hafla hiyo, RPC Masija amesema magari hayo ni jitihada za Serikali katika kuliwezesha Jeshi la Polisi kupata vitendea kazi vitakavyorahisisha utendaji wa majukumu yake ikiwemo kufanikisha usafiri na kufika kwa haraka kwenye maeneo ya matukio hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Aidha, RPC Masija ametoa pongezi na shukrani za dhati Kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na IGP Camillus Wambura kwa kuendelea kulipatia Jeshi la Polisi vifaa muhimu vya kazi.
Ameahidi magari hayo yatatumika kikamilifu kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, pamoja na kudumisha amani ya nchi.


0 Maoni