Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, amesema Jeshi hilo halitawavumilia watu wanaojificha chini ya mwavuli wa siasa ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kufanya vitendo vya uhalifu wakiwa na dhamira ya kuvuruga amani ya nchi.
Amesema watu hao wamekuwa wakitumia lugha za uchochezi na upotoshaji kwa lengo la kuigawa jamii, na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.
IGP Wambura ametoa kauli hiyo Agosti 11, 2025 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi unaofanyika Shule ya Polisi Tanzania- Moshi mkoani Kilimanjaro. Mkutano huo pamoja na mambo mengine unaolenga kujadili maendeleo, changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia uhalifu.
Katika hotuba yake, IGP Wambura alibainisha kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kukabiliana na uhalifu kwa kuimarisha mbinu za kiintelijensia, kuzuia matukio kabla hayajatokea kupitia dhana ya Polisi Jamii na kuongeza ushirikiano na wananchi.
Alisisitiza kuwa jeshi hilo halitavumilia mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vinavyolenga kuvuruga amani, huku akieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yanatokana na mshikamano wa ndani ya Jeshi na uungwaji mkono na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, IGP Wambura alisema Mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa maafisa waandamizi kutathmini utendaji kazi wa mwaka uliopita, kupanga mikakati ya kuhimili mabadiliko ya mifumo ya uhalifu, na kujadili hatua za kuimarisha usalama kuelekea uchaguzi mkuu ujao.


0 Maoni