NELSAP YABORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA WAKAZI WA RUSUMO KAGERA

Na Lydia Lugakila, Ngara.

Wakazi wa kijiji cha Rusumo wilayani Ngara Mkoani Kagera  mpakani mwa Tanzania na Rwanda, wametoa shukrani za pekee kwa Shirika la The Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program (NELSAP) kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hilo.


Wakazi hao, ambao hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika hospitali ya wilaya, wamesema kuanzishwa kwa Kituo cha Afya Rusumo kumewawezesha kupungua kwa gharama na muda waliohitaji kufuatilia matibabu.


Bi Rehema Musa, mmoja wa wakazi wa Rusumo, alielezea kwa masikitiko jinsi alivyokuwa akilazimika kusafiri hadi mkoani Mwanza kwa ajili ya kujifungua kipindi cha ujauzito wake, kutokana na kukosa uhakika wa huduma za matibabu katika kijiji chake. 


"Nlipokuwa nikiumwa, nilikuwa napanda pikipiki hadi Mshikamano kwa ajili ya matibabu sasa Nimefurahishwa na kuwepo kwa kituo karibu na nyumbani,” alisema Rehema.


Aidha, Damasi Justine aliongeza kuwa changamoto ilikuwa kubwa, hasa usiku, ambapo walilazimika kukodi gari kwa shilingi laki moja ili kufika hospitali ya wilaya kwa matibabu.


Kwa upande wake, Dr. Prisca Temba, mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Rusumo, alishukuru NELSAP kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vya matibabu, ambavyo vimeongeza ufanisi wa huduma katika kituo hicho.

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Rusomo Dr Prisca Temba

 "Kwa sasa tunatoa huduma zote za wagonjwa wa nje, kulazwa na upasuaji, na idadi ya wagonjwa inakua kwa kasi, wote wakihudumiwa ipasavyo," alisema Dr. Temba.


Mratibu wa NELSAP,  mhandisi Isack Alukwe, amesema kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazofaidika na mradi wa Rusumo, hususani kwa wakazi wa Ngara. 

Mratibu wa NELSAP, Eng Isack Alukwe

Aliongeza kuwa NELSAP imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika nchi za Afrika zinazopitiwa na bonde la Mto Nile, kwa ushirikiano na serikali za nchi wanachama.


Chapisha Maoni

0 Maoni