BY. JUSTINE MALILI ( MWANDAMIZI )
Ukipewa nusu shukuru, kisha anza na kuitafuta nusu iliyobaki kwa nguvu, akili na maarifa...kwa maana haipo mbali iko kwa mwenzako inakusubiri yule aliyepewa moja na nusu...
Ukipewa nzima amini una nusu ya mwenzako ambaye hana na ili mwenzako aipate nusu yake anatakiwa afanye kazi yako ili aichukue hiyo nusu yake iliyopo kwako...
Unapolalamika maisha ni magumu amini kuna mwenzako anatangaza ana pesa za kutosha benki na hazina kazi ya kufanya...
Ukilalamika kila siku wewe ni mtu wa kuugua na bado unadunda mtaani fahamu kuna mwenzako hivi sasa ni mwaka wa 7 hajawahi kuwa na maisha nje ya kitanda kwa maradhi yasiyokoma...
Ukiona una mtu wa kukushika mkono fahamu kuna mwenzako hana hata huo mkono wa kushikwa na bado anapambana na hali yake...
Siku zote mwanadamu huwa anapenda asivyovihitaji na anatamani visivyompenda...kuna mtu anatamani umaarufu lakini hana uwezo wa kumudu maisha ya umaarufu...na kuna mtu anatamani kuwa na pesa nyingi lakini hana uwezo wa kutunza pesa...
Kuna kijana anapenda mwonekano wa kitanashati halafu maisha yake na roho yake ni chafu...hujawahi kuona msichana anaazima nguo kwa rafiki yake ili akakutane COCO BEACH na mpenzi wake aliyeazima gari...? Simply wanatamani maisha wasiyoyaweza na wanapenda wasivyovimudu...
Kuna waliopewa masikio ili wasikilize na kujifunza na macho ili waone wanachojifunza ila inasikitisha kuona wanatumia masikio kusikiliza umbeya na wanatumia mdomo kutangaza vita...
Hata kichaa huwa anachagua kopo limpemdezalo jalalani haokoti kila kopo...ukichagua mdomo ufanye kazi ya kusambaza umbeya kuna mwenzako naye amechagua sikio lifanye kazi ya kusikiliza huo umbeya wako...na wote mnakuwa kijiji kimoja ila vitongoji ndiyo tofauti...
Kumbuka mwonekano wako wa nje ni taswira ya jinsi mwonekano wako wa ndani ulivyo...huwezi kusema wewe sio kahaba wakati unavaa mavazi yenye kusawiri maungo yako ya mwili...
Si kila kitu utajua kuna wakati utakuwa hujui kama vile ambavyo hujui kama wewe ni kahaba japo huuzi mwili...
Umaridadi huficha umaskini wa mwili ila hauwezi kuficha umaskini wa akili, mawazo na fikra...lakini pia hauwezi kuficha hali halisi ya maisha yako ya kimaskini...Smartness na utajiri huanzia kichwani na sio kwenye muonekano...
Ukiwa smart kichwani huna haja ya kutaka kututhibitishia kuwa wewe ni smart kwenye mwonekano wa mavazi...kwa sababu hutahiji tuone jinsi unavyovutia ila utahitaji tujifunze ni kwa namna gani ulivyo bora...
"Your first instinct is always right, so always go with your first instinct even if its a bad idea because bad ideas make good stories..."
☆Mwandamizi


0 Maoni