KYERWA YASHUHUDIA MAENDELEO MAKUBWA KATIKA SEKTA ZA ELIMU NA AFYA

Na Lydia Lugakila

Katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bahati Henerco ameonyesha pongezi kwa maendeleo yaliyofikiwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 akiiongoza Halmashauri hiyo.

Akiwasilisha ripoti hiyo katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo Bahati amesisitiza mikakati mizuri inayotekelezwa na Halmashauri ili kuboresha huduma kwa wananchi, pamoja na kupongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha amani na maendeleo katika taifa.

Amesema katika upande wa Elimu

ongezeko la madarasa na walimu vimeleta kicheko ambapo idadi ya madarasa imeongezeka kutoka 796 hadi 1,547, huku walimu wa shule za msingi wakiongezeka kutoka 1,089 hadi 1,147.


 Mwenyekiti huyo amesema fedha za elimu bila malipo zimepanda ambapo shule za sekondari zimeongezeka kutoka 23 hadi 33.


Bahati pia ameongeza kuwa vyumba vya madarasa vimeongezeka kutoka 237 hadi 414, na nyumba za walimu kutoka 23 hadi 61 huku ujenzi wa shule mpya, ikiwa ni pamoja na shule ya Ishaka katika kata ya Isingiro, unaendelea.


Amesema Shule za sekondari Umoja na Nyarutuntu pia zimefunguliwa na tayari zinatoa huduma.


Amesema zahanati ya Katera na kituo cha afya Nkwenda vimeboreshwa kusaidia kutoa huduma bora huku kituo cha afya Murongo kikiwa kimeanzisha huduma za kuhifadhi maiti.


"idadi ya vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka 26 hadi 34 pamoja na kiwango cha upatikanaji wa huduma za dawa na vifaa tiba kimepanda kutoka asilimia 80 hadi 90." alisema kiongozi huyo.


Ameongeza  ongezeko la mbolea za ruzuku limefikia tani 890 kutoka tani 380, huku vifaa vya kilimo kama magari na vipimia udongo vikitolewa.



Akizungumzia idadi ya vikundi vinavyonufaika na kilimo amesema imeongezeka kutoka 90 hadi 101 ambapo maafisa ugani wa mifugo pia wameongezeka kutoka 8 hadi 12, na vikundi vya wafugaji  kutoka 13 hadi 32.

Mwenyekiti Bahati Henerco amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Halmashauri katika kutekeleza mipango hiyo ya maendeleo. 

Aidha, amewapongeza viongozi wa serikali kwa jitihada zisizokoma za kuboresha elimu, afya, na kilimo katika Wilaya ya Kyerwa.

Kikao hicho kimeonyesha ufanisi wa Halmashauri katika kutekeleza mikakati ya maendeleo, ambapo ni muhimu kwa wananchi kutoa ushirikiano ili kufikia malengo haya kwa ufanisi zaidi.

Chapisha Maoni

0 Maoni