BY. JUSTINE MALILI ( MWANDAMIZI )
Unaweza kuwa umetilia mkazo sana kufikiria kuzalisha vitu vikubwa, kiasi cha kwamba unasahau hata kutunza na kufurahia kile ulichonacho sasa mkononi...
Kwa kawaida unatakiwa kuwa na furaha na mahali uliko, ukingojea kufika kule mahali ambapo unataka kupafikia...
Kuna mambo mawili muhimu sana ambayo unatakiwa kuwa nayo, SUBIRA na UVUMILIVU....Uvumilivu na subira ndiyo ushindi katika njia za mafanikio ya maisha ya mwanadamu...
Usichokijua ni kwamba, Binadamu huwa tunatumia muda mwingi maishani mwetu tukingojea (tukisuburi) kuliko muda tunaotumia kupokea...na siku zote mara baada ya kupokea tulichokuwa tunakingojea, basi huwa tunaanza kungojea tena kitu kingine kipya...
IKO HIVI...
Baada ya kupanda Mkulima yeye huendelea kuishi maisha yake ya kawaida kila siku, akingoja shamba lake lijae mimea iliyochipuka kwa kadiri ya anavyotarajia...mkulima hawezi kulazimisha kuvuna mazao ambayo hayajakomaa, bali husubiria mazao yakomae ndipo apate kuyavuna...
Leo hii ni mwaka 2025 ila toka mwaka 2015 watumishi wa serikali wanangojea tamko la rais na serikali kuhusu nyongeza ya mshahara, na ikitokea wamepatiwa nyongeza ya mshahara watangojea tena siku nyingine ya kuongezewa mshahara upya...huwachukua muda mfupi sana kufurahia nyongeza ya mshahara waliyopatiwa kuliko muda wanaosubiria kupata nyongeza ya mshahara...
Hivi sasa kuna anayengojea kupata mtoto kwa hamu kubwa na akishapata mtoto, ataanza kungojea mtoto huyo aache kuvaa nepi ama pampass na kisha aanze kuvaa suruali ndefu au gauni refu akiwa amekua...
Na kadiri muda utakavyozidi kwenda mzazi huyo huyo ataanza kungoja tena muda wa mtoto kuanza kujinunulia suruali au gauni kwa pesa yake yeye mwenyewe na sio tena kwa pesa ya mzazi...
Unangoja kununua nyumba, kisha unaanza kungoja tena kununua vyombo vya ile nyumba ambayo huingojei tena...
Kwahiyo...??
Jifunze kufurahia kungoja, ama kuwa na subira na uvumilivu, na huku ukifahamu kuwa subira na uvumilivu ndivyo vitakavyo kufikisha katika ndoto yako na matarajio yako...
Watu waliokosa subira na uvumilivu mara nyingi huwa hawafiki mwisho wa safari waliyoianzisha, kwa maneno mepesi na rahisi kabisa ni kwamba, mara nyingi huwa hawakamilishi ndoto zao...
Kuna usemi mmoja unasema "Cha haraka ni dhaifu, na cha pole pole ni kizima kama kigongo..." msemo huu una maana ya kwamba, chochote kinachofanywa kwa haraka huwa kinawafaa wale wasio na subira wala uvumilivu na wale wasio na uwezo wa kungoja vyema...
Na upo uwezekano mkubwa hicho wanachokitaka kwa haraka kisidumu kwa sababu walikitaka kikiwa bado hakijakamilika...Lakini wale wenye subira na uvumilivu na wale walio tayari kungojea wakati ulioteuliwa na Mungu ufike ndipo wakipokee, basi kitu hicho kitaundwa sawa sawa na kitakuja kuwa ni cha kudumu kwa muda mrefu...
Kwanini kitadumu, kwa sababu kitakuja kikiwa kimeshakamilika na kwa wakati sahihi bila kulazimisha...hivyo hata siku moja usilazimishe fungu lako sasa, wakati bado halijawa tayari.
Usilazimishe ndoto zako unazoota kila siku zikamilike leo wakati MUNGU anasema kesho kwa maana bado anazitengeneza...Iko wazi siku zote mtu mwenye haraka hula chakula kibichi, na mwenye subira na uvumilivu hula chakula kilichoiva...
Usiwe na haraka ya maisha utakula chakula kibichi...subiri wakati wako unakuja ili ule chakula kitamu na kilichoiva...
Usione unachelewa kwa sababu hakuna aliyewahi...hao unaowaona wakikupita na kukuacha nyuma wakati mna umri sawa na yamkini wengine umewazidi na miaka, tambua huo ndiyo wakati wao sahihi waliopangiwa na MUNGU kuvuna walichopanda...
Kama wakati wako bado wewe kuwa na subira na uvumilivu ukitambua wakati wako waja...haijalishi itakuwa ni lini lakini amini wakati ulio bora unakuja na uko njiani...Be humble...!! Ongeza bidii na jitihada, weka nia na jiandae kupokea yaliyo bora na mema...
"Overcome your barriers, intend the best, and be patient. You will enjoy more balance, more growth, more income, and more fun.."
☆Mwandamizi

0 Maoni