TATIZO SIO KAZI TATIZO NI AJIRA ( KONA YA MWANDAMIZI )

                                                                                                                      By. Justine Malili ( Mwandamizi)

Siku zote mtu aliyeajiriwa hana mamlaka wala uwezo wa kujiongezea kipato kupitia mshahara isipokuwa yule aliyemwajiri pekee..ila mtu aliyejiajiri ana uwezo na mamlaka ya kujiongezea kipato...

Mtu aliyeajiriwa anauza muda wake na nguvu zake kwa gharama ndogo kwa ajili ya kukidhi haja zake kwenye maisha yake, na huku akifanya kazi kubwa na kutumia muda mwingi  kutimiza ndoto za mwajiri wake...

Waajiri wote wana sifa moja na sifa yao kuu ni kununua muda na nguvu za wafanyakazi wao na kuwalipa fedha zitakazoweza kuendesha maisha yao na sio kutimiza malengo yao...

Mwajiriwa unayetegemea mshahara kumbuka mshahara wako pekee hauwezi kukufanya ujitegemee kiuchumi... 


Na kuongeza elimu yako ili uongezewe mshahara kwa kudhani unapoongezewa mshahara ndipo unaweza kujitegemea kiuchumi ni ukosefu wa maarifa...

Leo hii watu wengi bado wanafikra ya kuwa  unapopandishwa cheo kazini au kuongezewa mshahara unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya maendeleo...

Ni vizuri kuwaza hivyo ila fahamu ya kwamba kabla wewe hujalipwa mshahara tayari mwajiri wako alishapiga hesabu ni kiasi gani cha pesa kitakachotosha kufanya wewe uishi na kuisaidia familia yako na sio kutimiza malengo yako...

Ikiwa wewe ni mwajiriwa mahala fulani na unategemea mshahara wako kutimiza malengo yako Usipambane kuongezewa mshahara na marupurupu na huku ukitaka upunguziwe masaa ya kufanya kazi na kuongezewa siku za mapumziko...

Bali pambana kuhakikisha unaondoka kwenye mikono ya kutimiza malengo ya mwajiri wako...ili uweze kutimiza malengo na ndoto zako...

Na kama ukishindwa basi hakikisha unatengeneza kipato binafsi nje ya ajira yako...ili kuwa na uchumi imara na bora...

Kanuni inasema ili uweze kujitegemea kiuchumi unatakiwa kutoa zaidi ndipo upokee zaidi, usitoe muda wako na nguvu zako nyingi kwa mtu, bali tumia muda wako na nguvu zako nyingi kwenye kusaidia watu wengi kwa kutatua matatizo yao ili wakupe pesa...

Malalamiko au chuki kwa mwajiri kwa kuwa hapandishi vyeo na wala haongezi kima cha chini cha mshahara ni jambo la kawaida kwa waajiriwa wote wanaomini ndoto zao zitakamilika kwa mshahara kama ilivyo kawaida kumkuta Paroko kashika Biblia...

Fanya kazi mahala ulipoajiriwa kwa malengo ya kuja kujiajiri siku za usoni. Na usifanye kazi sehemu uliyoajiriwa ukifikiri mshahara mnono na marupurupu lukuki yataweza kukamilisha ndoto zako...

Kumbuka faida ni bora kuliko mshahara kwa maana mshahara utafanya kazi ya kukufanya uishi,  na faida itafanya kazi ya kukupeleka kwenye malengo na ndoto zako...

"Do not work for Money instead you have to dedicate your life to the service of others...The more you serve the more effective you become..." 

☆Mwandamizi

Chapisha Maoni

0 Maoni